Mara nyingi huwa napenda kula ubwabwa na njegere, sijui kama na wewe mwenzangu unapenda kula njegere? Kama jibu ndiyo basi nakusihi uungane nami katika makala haya ili uweze kujifunza namna ya kulima kilimo hiki.
Nakusihi kulima kilimo hiki kwa kwa sababu , kilimo cha njegere ni kilimo chenye tija kwa wakulima. Njegere ni mbegu za spishi za mimea katika jamii ya kunde ambayo hukuzwa sehemu mbalimbali duniani katika maeneo ya ukanda wa juu.
Spishi kadhaa za njegere ni:
1. Njegere kubwa (chickpea)
2. Njegere ya kizungu (common pea)
3. Njegere sukari (snow pea and snap pea)
Hapa nchini Tanzania njegere hulimwa nyanda za juu kusini, nyanda za juu kaskazini na kwenye miinuko ya Usambara na Uluguru. Katika ulimwengu njegere hulimwa kwa wingi katika Asia ya kati, Mediterania na Afrika ya kaskazini.
Kuna aina mbalimbali za njegere zinazopatikana Tanzania kama Tanganyika yellow, Idaho white, Rondo na Mbegu za kienyeji.
HALI YA HEWA:
Kwa tafiti inaonesha zao la njegere hustawi vizuri maeneo yenye hali ya ubaridi wa sentigredi 17 – 21 C, na mwinuko zaidi ya mita 1200 usawa wa bahari na mvua, unyevu wa kutosha na maji yasiyotuama. Udongo uliowekwa mbolea, kulimwa kwa kina na wenye tindikali ya PH 5.5 – 6.5.
UTAYARISHAJI WA SHAMBA:
Maandalizi yanatakiwa yaanze kabla msimu wa mvua haanza, Shamba / bustani itayarishwe kwa trekta au pawatila au jembe la mkono au jembe la ng’ombe kwa kufuata mahitaji ya udongo kama kutotuamisha maji, kulimwa kwa kina. Changanya mbolea za asili (samadi au mboji) na udongo ili kurutubisha ardhi.
UTAYARISHAJI WA MBEGU
Chambua mbegu nzuri zinazoonekana hazina matatizo, zilizo na afya ili kupata mazao mengi. Unashauriwa kuandaa mbegu mapema ili kuweka maandalizi mazuri.
UPANDAJI.
Njegere hupandwa kipindi cha mvua ama kwa umwagiliziaji, maana udongo unatakiwa uwe na unyevu ili kufanya mmea kukua vyema, nafasi za kupanda:-
i) 60 sm – 90 sm x 5.7 sentimita kwa mbegu fupi.
ii) 12 sm – 15 sm x 5 – 7.5 sentimita katika safu mbili za sentimita 90 kwa mbegu inayotambaa.
iii) Njegere hustawi vizuri zikipata sehemu za kutambalia.
iv) Mbegu ya njegere huota baada ya siku 7 – 10.
MBOLEA.
Ukitumia mbolea za asili (samadi au Mboji) njegere hustawi vizuri. Katika kipindi cha ukuaji ni muhimu kuweka mbolea ya chumvichumvi za nitrogen kwa kipimo cha kg 40 kwa hekari.
UPALILIAJI
Njegere zipaliliwe zikiwa changa shamba lililotayarishwa vizuri na kuondolewa magugu ya mda mrefu (Perrenial weeds) linaweza kupalliwa mara moja, kwa sababu njegere hukua haraka, na zinaweza kushindana na magugu. Baada ya kutoa maua, njegere zisipaliliwe ili kuongeza mazao.
Magugu hushindana na kunyanganyana na mimea kutumia virutubisho. Pia huongeza kivuli wakati wa utoaji maua na kusababisha upungufu mkubwa wa mazao. Palizi hufanyika kwa mkono au kutumia dawa za kuua magugu.
MAGONJWA & WADUDU
MAGONJWA.
Ascochyta.
Kutokea kwa mabaka makubwa ya kahawia kwenye majani na matunda. Pia hutokea hata kwenye shina. Katikati ya baka huwa rangi ya kijivu, kingo nyekundu / nyeupe husababishwa na fangasi aina ya Ascochyta pisi.
Root Rot na Blight disease.(kuoza kwa mizizi na Blingt)
Husababishwa na fangasiA. pinodella na mycosphaerella pinodes.
Dalili: – madoa madogomadogo yenye rangi ya zambarau / rangi ya kahawia iliyokaza au madoa meusi ambayo huungana na kusababisha jani na maua kuwa yenye rangi nyeusi .
Kuzuia.
1. Kutumia mbegu zisizo na magonjwa.
2. Kuzika mabaki ya mazao yaliyoadhirika kwa miaka 3 – 4.
Downy mildew.
Husababishwa na fangasi Erysiphe polygoni.
Dalili: Majani kuonekana kama yamemwagiwa unga na baadae na
kufa. Ugonjwa unaathiri zaidi mimea kipindi cha uhaba wa
unyevunyevu.
Kuzuia: – Kutumia sulphur ya unga kama inavyoshauriwa.
Fusarium wilt:– Husababishwa na fangasi / ukungu Fusarium oxysporum.
Dalili:
1. Majani kubadilika rangi kuwa manjano.
2. Mimea kudumaa.
3. Ugonjwa ukitokea kwenye mimea michanga huua mmea wote.
Kuzuia: – Tumia mbegu yenye uvumilivu kwa ugonjwa huu.
Virusi – Mmea huonekana kuwa na uvimbeuvimbe kuzunguka jani. Mmea hudumaa.
Kuzuia: – Kutumia mbegu zisizo na maradhi.
WADUDU
Wapo wadudu wengi ambao hushambulia zao la njegere. Baadhi ni kama American bollworm, Bean flies, Bean Aphids, Pea Aphids huambukiza virusi na Green peach aphids.
Inashauriwa kumwona mtaalam wa kilimo aliye karibu yako kwa ufafanuzi wa kuwazuia wadudu waharibifu.
UVUNAJI
Kwa njegere teke / mbichi hukomaa siku 60 – 90 na kwa njegere kavu huchukua siku 80 -150 kukomaa . Njegere teke huvunwa punje zikiwa bado mbichi, Uvunaji hufanyika mara 2 – 3 kwa wiki wakati wa kipindi cha ukuaji. Zaidi ya kilo 3000 kwa hekta za njegere teke huvunwa, Njegere kavu huvunwa wakati punje zimekauka na kuwa ngumu na ni muhimu kuwahi kuvuna njegere kavu ili kutopoteza mavuno zikipasuka. Mavuno ya punje kavu na kilo 1500 kwa hekta.
asante sana kwa kusoma makala haya
0 Comments