UFUGAJI BORA WA KAMBALE

Kambale (Ietalurus Punetaus), ni aina ya samaki ambao wana majina mengi kulingana na eneo na jamii husika. Samaki hawa unaweza kusikia wakitajwa kwa majina mengine kama vile, kambale channel, koleo, samaki kidevu Na kuendelea.
     Asili ya Kambale
Asili ya samaki hawa ni Amerika ya Kaskazini. Samaki hawa hukua kwa haraka sana, na kuwa na uzito mkubwa. Aina hii ya samaki hupendwa na watu wengi kwa kuwa nyama yake ina ladha nzuri na ni laini sana.

Samaki hawa huzaliana vizuri zaidi wanapokuwa mtoni au sehemu ambayo wanapata tope. Mfugaji anapokusudia kufuga aina hii ya samaki kibiashara, ni lazima kusakafia bwawa ili kuepuka uharibifu unaoweza kusababishwa na samaki hawa.
     Umbile lake
Samaki aina ya kambale wana umbo refu, pia ni wapana kuanzia shingoni, ingawa kichwa ni kidogo, na upande wa mkia ni mwembamba. Samaki hawa wana rangi ya kijivu na wengine nyeusi.

Jinsi ya kulisha kambale
Unaweza kulisha kambale kwa kutumia unga wa samaki, maharagwe yaliyosagwa, mahindi, mchele pumba, ngano na bidhaa nyingine. Unaweza kujenga mfumo ambao utawawezesha samaki hawa kupata aina mbalimbali za wadudu, pamoja na majani, ili kusaidia wapate mlo kamili.
     Ukuaji na uvunaji wa kambale
Aina hii ya samaki, wakitunzwa vizuri, wanaweza kukua kwa haraka na kuwa na uzito mzuri unaoweza kumpatia mfugaji faida nzuri. Unaweza kuanza kuvuna kambale baada ya miezi sita tangu walipopandikizwa kwenye bwawa.
     Soko la kambale
Fikiria soko la samaki kabla ya kuanza kuzalisha.
Wafugaji walio wengi, wamekuwa wakianzisha miradi ya ufugaji wa samaki kwa kufuata mkumbo bila kutambua kwanza soko watakalozalishia samaki hao. Jambo hili huwafanya wafugaji kuwa na kipato kidogo tofauti na nguvu waliyotumia kuzalisha.
Inapofikia wakati wa kuvuna samaki, kiasi kikubwa huuzwa papo hapo bila kufika kwenye soko halisi, jambo linalosababisha kipato kuwa duni. Ni vyema mfugaji akawa na soko maalumu ambalo atazalishia. Unaweza kuzalisha kwa ajili ya shule, hospitali, vyuo, au taasisi yoyote. Halikadhalika jamii inayokuzunguka na taasisi nyinginezo.

       Mambo ya kuzingatia kabla ya kufuga samaki
• Fahamu ni aina gani ya samaki inayopendwa zaidi katika eneo ulipo.
• Samaki wanaopendwa wanatakiwa wawe na ukubwa gani.
• Kiasi cha samaki kinachohitajika katika soko ulipo.
• Ni kipindi gani ni kizuri kwa uvunaji wa samaki.
• Ni wakati gani mzuri wa kuuza samaki.
• Je, katika eneo lako kuna mfugaji mwingine anaezalisha samaki kwa ajili ya soko hilo?.
• Bei ya aina ya samaki unaozalisha ikoje?
      Wasikilize wateja
Wakati wote mfugaji anapouza samaki, ni lazima kusikiliza kwa umakini, wateja wako wanasemaje.
• Je, wanapendelea samaki unaouza.
• Je, samaki wako ni wadogo sana au ni wakubwa sana.
• Wakija kununua wananunua kwa kiasi gani, kikubwa au kidogo.
• Je, wanapendelea uzalishe zaidi?
• Je, kuna wafanyabiashara wanataka uzalishe zaidi ili nao wanunue.
• Wanataka samaki wawe kwenye ubora gani.
• Wanaridhika na bei unayowauzia.
      Fuata haya kwa ufanisi wa soko la samaki
• Hakikisha samaki wako katika hali ya usafi na vyombo salama unapovua tayari kwa kupeleka sokoni.
• Samaki ni bidhaa inayoharibika kwa haraka, hivyo hakikisha unawapeleka sokoni mara tu baada ya kuwavua.
• Hakikisha gharama za usafiri, utunzaji na uhifadhi, zinalipwa kutokana na bei ya soko.
• Kumbuka gharama za uhifadhi wa bidhaa inayoharibika haraka kama samaki ni kubwa, hivyo vua kwa awamu kulingana na mahitaji.
• Unaweza kuongeza thamani ya samaki kwa kufanya mambo ya msingi yanayohitajika kwenye uandaaji wa samaki, kama vile kuparua na kutumbua.
• Unaweza kuwasafisha, na pia kuwakaanga kulingana na soko husika.
Kwa kuzingatia mambo hayo machache, mfugaji anaweza kufanya maamuzi sahihi kabla ya kuwekeza kwenye mradi wa ufugaji wa samaki. Pia ni muhimu kuzingatia mahitaji muhimu ya ufugaji wa samaki, ili kuepuka gharama zisizo za lazima.


     Tengeneza chakula cha samaki mwenyewe
Mfugaji anaweza kupunguza gaharama za kununua chakula kwa ajili ya samaki, kwa kutengeneza chakula mwenyewe kwa kutumia malighafi ulizo nazo katika eneo lako. Tumia resheni rahisi ambayo itakupatia chakula cha kutosha na kwa gharama nafuu.
Mahitaji
• Pumba ya mahindi sadolini 1.
• Pumba ya ngano au mpunga sadolini 1.
• Dagaa sadolini 1.
• Kilo moja ya soya.
• Robo kilo ya mashudu ya pamba au alizeti.
Namna ya kuandaa
• Changanya malighafi hizo kwa pamoja.
• Saga hadi zilainike.
• Kanda kama vile unga wa kutengenezea chapati.
• Weka kwenye mashine ya kusaga nyama au kutengenezea tambi.
• Anika kwenye jua la wastani.
• Baada ya kukauka, vunja vunja kwenye vipande vidogo vidogo hasa kwa kuzingatia umri wa samaki unaokusudia kuwalisha.
• Tumia lishe hiyo kwa samaki mara tatu kwa siku.

0 Comments